Takukuru yaagizwa kumkamata mhandisi wa maji Mkoani Kagera

0
813

Naibu Waziri wa Maji Juma Aweso ameliagiza Jeshi la Polisi pamoja na Taasisi ya kupambana na kuzuia  Rushwa nchini  Takukuru wilayani Muleba mkoani Kagera, kumkamata na kumhoji Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba Boniphace Lukoo pamoja na mkandarasi kampuni ya Sajac Investment aliyehusika katika ujenzi wa mradi wa Maji wa Katoke.

Naibu Waziri Aweso amechukua hatua hiyo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi wa Katoke ambao wamedai hawajawahi  kupata huduma ya maji  tangu  mradi huo ulipokabidhiwa mwaka 2016 huku mkandarasi akiwa kalipwa shilingi milioni mia nne na nne kati ya milioni mia nne sabini na sita ambazo ni gharama ya mradi wote.

Changamoto ya uhaba  wa Maji imekuwa ikiwakabili  wakazi zaidi ya elfu tatu na mia mbili na arobaini na watano wa kata ya Katoke yenye vijiji viwili vya Katoke na Kahumulo .

Pia  Naibu Waziri Aweso amepiga marufuku mkandarasi huyo kampuni ya Sajac Investment kupewa kazi yoyote ya ujenzi wa miradi ya maji iliyo chini ya wizara hiyo.