Naibu Waziri wa Maji Juma Aweso ameliagiza Jeshi la Polisi pamoja na Taasisi ya kupambana na kuzuia Rushwa nchini Takukuru wilayani Muleba mkoani Kagera, kumkamata na kumhoji Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba Boniphace Lukoo pamoja na mkandarasi kampuni ya Sajac Investment aliyehusika katika ujenzi wa mradi wa Maji wa Katoke.
Naibu Waziri Aweso amechukua hatua hiyo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi wa Katoke ambao wamedai hawajawahi kupata huduma ya maji tangu mradi huo ulipokabidhiwa mwaka 2016 huku mkandarasi akiwa kalipwa shilingi milioni mia nne na nne kati ya milioni mia nne sabini na sita ambazo ni gharama ya mradi wote.
Changamoto ya uhaba wa Maji imekuwa ikiwakabili wakazi zaidi ya elfu tatu na mia mbili na arobaini na watano wa kata ya Katoke yenye vijiji viwili vya Katoke na Kahumulo .
Pia Naibu Waziri Aweso amepiga marufuku mkandarasi huyo kampuni ya Sajac Investment kupewa kazi yoyote ya ujenzi wa miradi ya maji iliyo chini ya wizara hiyo.