Mkuu wa mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Marco Gaguti ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) mkoani humo, kuchunguza mradi wa ujenzi wa hospitali ya halmashauri ya mji wa Nanyamba kutokana na kuwepo kwa usiri na wajumbe wa kamati ya ujenzi kutoshirikishwa kwenye ununuzi wa vifaa.
Brigedia Jenerali Gaguti ametoa agizo hilo baada ya kutembelea hospitali hiyo na kupata malalamiko kutoka kwa baadhi ya wajumbe hao wa kamati kuwa, hawajashirikishwa kwa jambo lolote na wanapojaribu kuhoji hawapatiwi majibu stahiki kutoka kwa uongozi wa halmashauri hiyo.
Wajumbe hao wamesema kazi yao kubwa ni kupokea vifaa vya ujenzi na wanapotaka kufanya kikao na Wasimamizi wakuu wa mradi huo imekuwa ikishindikana.
Akizungumza na wakazi wa mji wa Nanyamba, Brigedia Jenerali Gaguti amesema baada ya uchunguzi wa TAKUKURU kukamilika, Watendaji watakaobainika kufanya ubadhirifu katika mradi huo wa ujenzi wa hospitali ya halmashauri ya mji wa Nanyamba watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Amewataka Watendaji wa mkoa wa Mtwara kukamilisha usimamizi wa miradi kwa wakati na kuweka mbele maslahi ya Taifa, ili miradi hiyo iwe na manufaa kwa Wananchi.