Tafiti zabainisha uwekezaji makuzi ya watoto bado mdogo

0
477

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalumu, Dkt. Dorothy Gwajima amesema tafiti mbalimbali zilizofanyika barani Afrika zimebaini kuwa uwekezaji kwenye malezi na makuzi ya watoto wadogo bado ni mdogo.

Amesema uwekezaji huo huenda haujafanywa vizuri katika ngazi ya familia, kwani jamii haijafanikiwa kuwapeleka watoto kwenye huduma za afya kama inavyotakiwa japokuwa huduma hizo zimesogezwa karibu na jamii.

Vilevile inawezekana pia uwekezaji huo sio mzuri kwenye upande wa elimu japokuwa shule zipo karibu kwenye jamii na kwamba inawezekana pia uwekezaji huo sio mzuri kwenye lishe japokuwa kwenye mikoa nchini wakulima wanaendelea kulima vyakula mbalimbali.

Amesema uwekezaji kwenye usalama wa watoto bado pia sio mzuri kwa kuwa baadhi ya mila na tamaduni kandamizi zimepewa tija kwenye malezi na makuzi ya watoto kwenye jamii, jambo ambalo sio sawa.

Aidha ameongeza kuwa kutokana na uwekezaji huo kutokuwa na uwiano ulio sawa kama inavyotegemewa na endapo hali hiyo ikiendelea hivyo wataandaliwa watoto na hatimae kuwa na nguvu kazi isiyo na tija kwenye mataifa ya Afrika.