TACRI Kuzalisha miche Milioni 20 ya kahawa

0
139

Serikali imejipanga kuzalisha miche ya kahawa milioni 20 kupitia wadau mbalimbali wakiwemo Bodi ya Kahawa, Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TACRI) na Sekta binafsi.

Hayo yamesemwa leo tarehe 02 Julai, 2022 na Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde alipotembelea Makao Makuu ya TaCRI yaliyopo kata ya Lyamungu, Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro.

“Sote tunafahamu kuwa kahawa ni moja ya zao la kimkakati, hivyo Wizara tumeweka mkakati wa kuongeza uzalishaji wake ambapo hatua ya awali ni kuongeza uzalishaji wa miche bora ambayo ina ukinzani wa magonjwa na tija kubwa kwa wakulima.

“Naitaka TACRI pamoja na kuendelea kuongeza uzalishaji wa miche bora, lakini pia mjikite katika kutoa elimu kwa wakulima juu ya miche hiyo na mbinu bora za kufuata ili waweze kuzalisha kahawa kwa tija na kuongeza kipato chao”Amesema Mavunde

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa TACRI, Dkt. Deusdedith Kilambo, aliishukuru Serikali kwa kuongeza bajeti yao kutoka milioni 328 mwaka 2021/2022 hadi milioni 800 mwaka 2022/2022 na kusisitiza kwamba TaCRI wamejipanga kuhakisha lengo la kuzalisha miche bora milioni 20 kwa mwaka 2022/2023 linafikiwa.