Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameziagiza wizara, taasisi, mashirika yote ya umma binafsi pamoja na vikundi vya uzalishaji zinazotumia nishati ya kuni na mkaa zianze kutumia nishati mbadala kwa kupikia na shughuli nyingine za uzalishaji.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo jijini Dodoma, wakati akitoa tamko kuhusu wiki ya Mazingira Duniani.
Amesema kuwa taasisi kama shule, vyuo, hospitali na majengo makubwa zinapaswa kuzingatia ufungaji wa mifumo ya nishati ya gesi kwa ajili ya kupikia.
“Kila wizara ifanye ufuatiliaji kwenye taasisi zake na nipatiwe taarifa ya hali ya utekelezaji kila baada ya miezi sita inayoonesha ni taasisi ngapi zimefikiwa, zimebadili mifumo au zimejenga majengo kwa kuzingatia hitaji la nishati mbadala,” ameagiza Waziri Mkuu Majaliwa.
Kadhalika, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka Viongozi wa jiji la Dodoma kuhakikisha wanaweka mkakati, ili maeneo yote yanayopimwa yapandwe miti na kila anayepata kiwanja aelimishwe kuhusu umuhimu wa kupanda miti.