Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amewataka maafisa habari wa taasisi za serikali kuhakikisha taasisi zao zinatenga bajeti kwa ajili ya utayarishaji wa vipindi vyenye ubora vitakavyorushwa kwenye televisheni na redio ili wananchi wafahamu serikali inafanya nini.
Akimwakilisha Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, katika ufunguzi wa mkutano wa mafunzo kwa watayarishaji wa vipindi vya elimu kwa umma, Msigwa amesema serikali inatambua mchango wa taasisi hizo katika kuelimisha umma.
Msigwa amesema baadhi ya taasisi hazitengi bajeti ya kutayarisha vipindi na hivyo wakati mwingine kurusha vipindi vilivyo chini ya kiwango.
Aidha, ameipongeza TBC kwa kuboresha vipindi vyake na kusema kuwa kumekuwa na watazamaji wengi na ndio maana Serikali inatumia TBC kutoa taarifa za Kazi za Serikali na kutangaza miradi ya kimkakati ye Taifa na maendeleo kwa ujumla.
Akitoa ushauri kwa TBC, Msigwa ameishauri ianzishe habari ya Kingereza ambayo itasaidia kutangaza mambo mazuri ya Tanzania ikiwepo kutangaza utalii na fursa za uwekezaji ili kuleta wageni wengi zaidi.
TBC imeandaaa mkutano wa 106 wa mafunzo ya uandaaji wa vipindi vya televisheni, redio na mitandao ya kijamii mkoani Iringa ambayo yanatolewa kwa maofisa wa habari wa wizara, taasisi, mashirika ya umma, idara na halmashauri.