Taasisi za fedha zatakiwa kuwaamini wachimbaji wadogo

0
245

Taasisi za fedha nchini zimetakiwa kuendelea kuwaamini na kuwakopesha wachimbaji wadogo wa madini.

Waziri wa Madini Dotto Biteko amesema hatua hiyo itawasaidia wachimbaji hao kuongeza tija na mitaji, ili kuendana na kasi ya teknolojia kwenye shughuli za uchimbaji madini.

Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi rasmi wa maonesho ya tano ya kitaifa ya teknolojia ya madini yanayoendelea mkoani Geita na kuongeza kuwa, lengo la serikali ni kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini kukuza mitaji yao na kuwa wawekezaji wakubwa ndani ya nchi yao.

Aidha Waziri Biteko amewapongeza wanawake kwa kujitokeza kwa wingi kwenye shughuli za uchimbaji na biashara ya madini na kuendelea kutoa wito kwa wanawake zaidi kuwekeza kwenye sekta hiyo inayokuwa kwa kasi nchini.

Pia amesisitiza utunzaji wa mazingira kwa wawekezaji na wachimbaji wadogo wa madini, ili kuendelea kunufaika na biashara hiyo bila kuleta madhara katika jamii.

Maonesho hayo ya tano ya kitaifa ya teknolojia ya madini yanajumuisha wadau wa sekta ya madini kutoka nchi za Uganda, Zambia na Burundi na yanaendelea hadi tarehe 8 mwezi huu katika viwanja vya ukanda wa uwekezaji (EPZ) Bombambili mkoani Geita.