Rais Samia Suluhu Hassan ameziagiza taasisi za fedha nchini kujadili na kutoa mapendekezo ya haraka kwa Serikali, ya namna ya kuimarisha uchumi ulioporomoroka kutokana na janga la UVIKO – 19.
Rais Samia ametoa agizo hilo jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa 20 wa taasisi za fedha nchini, ulioandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Pia amezitaka taasisi hizo za fedha nchini kujadiliana na kuandaa mikakati haraka iwezekanavyo, itakayosaidia kupunguza umaskini nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba amezitaka benki za biashara nchini kuongeza ubunifu na kupeleka wizarani mapendekezo ya kisera, ili wizara hiyo iweze kuongeza utoaji wa mikopo kwenye sekta binafsi hasa katika maeneo makubwa kiuchumi.
Kauli mbiu ya mkutano huo wa 20 wa taasisi za fedha nchini uliojumuisha wadau wa masuala ya fedha kutoka ndani na nje ya nchi ni “Ukuaji wa uchumi endelevu wakati na baada ya UVIKO – 19, vipaumbele na sera mbadala”.