Taasisi ya PCMC Health Care yawatembelea wagonjwa Vijibweni

0
2026

Wakazi wa manispaa ya Kigamboni jijini Dar es salaam wameipongeza serikali kwa kufanya maboresho katika sekta ya afya, hasa huduma za mama na mtoto na hivyo kuwawezesha akina mama wengi kuwa na uhakika wa kujifungua salama.

Wakizungumza na Mwandishi wa TBC katika hospitali ya wilaya ya Kigamboni,- Vijibweni, walipotembelewa na Taasisi ya Madaktari bingwa ijulikanayo kama PCMC Health Care Limited, baadhi ya akina mama waliojifungua na wanaosubiria kujifungua hospitalini hapo wamesema kuwa uwajibikaji miongoni mwa wahudumu wa afya na upatikanaji wa dawa katika hospitali na vituo mbalimbali vya afya ni wa kuridhisha.

Madakari na wahudumu wa afya kutoka Taasisi hiyo ya PCMC Health Care Limited yenye makazi yake jijini Dar es salaam wamewajulia hali wagonjwa waliolazwa katika wodi ya wazazi na watoto katika hospitali ya Vijibweni ikiwa ni moja ya njia ya kuonyesha upendo.
Kiongozi Mkuu wa Taasisi hiyo Richard Ulanga amesema kuwa suala la utoaji wa huduma za afya ni mtambua, hivyo halipaswi kuachiwa serikali pekee bali wadau wote wanatakiwa kushirikiana na serikali ili kufanikisha jambo hilo.

Ameongeza kuwa lengo la Taasisi hiyo ya PCMC Health Care Limited ni kutoa huduma bora za afya kwa Wananchi kwa kushirikiana na serikali.

Kwa mujibu wa Ulanga, kila mwaka taasisi hiyo imekua ikifanya matendo ya kihuruma ya utoaji huduma za upimaji afya bila malipo, kutembelea vituo mbalimbali vya watoto yatima, kutembelea wagonjwa waliolazwa katika hospitali mbalimbali na kuwapatia zawadi za aina tofauti.

Kwa upande wake Katibu wa afya wa hospitali hiyo ya wilaya ya Kigamboni,- Vijibweni, Bernard Makupa amesema kuwa pamoja na kujitahidi kutoa huduma bora za afya, lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya idadi kubwa ya wagonjwa hasa wajawazito wanaofika hospitalini hapo kujifungua.

Nao baadhi ya akinana waliojifungua wamesema wamewashukuru madaktari na wauguzi wote kwa huduma nzuri waliyoipata.

Hospitali ya Vijibweni inazalisha wastani wa akina mama kumi hadi kumi na Watano kwa siku, ikiwa ni wastani wa akina mama Mia Tatu kwa mwezi.