Waandamanaji wanaoipinga serikali ya mpito ya kijeshi nchini Sudan bado wako nje ya Makao Makuu ya jeshi la nchi hiyo, wakishinikiza uongozi wa kijeshi kurejesha utawala wa kiraia na kufuata matakwa ya wananchi.
Waandamanaji hao wameahidi kuendelea na maandamano yao hadi hapo jeshi litakapowarejeshea mapinduzi yao.
Wamedai kuwa Jeshi la Sudan limeteka maana ya maandamano yao, kwani walimtoa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Omar Al Bashir madarakani ili kupata utawala mpya wa kiraia na sio utawala wa kijeshi unaowakandamiza na kuendeleza utawala wa Al Bashir.
Licha ya viongozi wa serikali ya mpito nchini Sudan kuahidi kuwaachia watu kadhaa waliokuwa wakishikiliwa wakiwemo askari walioshiriki katika maandamano hayo, bado waandamanaji wanasema hawajaridhika.
Waandamanaji pia wanataka jeshi la nchi hiyo kuondoa vizuizi vilivyowekwa barabarani ili kutekeleza tangazo lilitolewa kuwa limeondoa hali ya tahadhari iliyokuwa imewekwa kwa muda wa miezi mitatu.