Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ameagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kuandika andiko la kuomba fedha za ujenzi wa mradi wa soko la mazao na stendi ya mkoa.
Chongolo ameyasema hayo katika kijiji cha Msanyila wilayani Mbozi mkoani Songwe alipokuwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya maendeleo.
Aidha, amesema kujengwa kwa soko la mazao wilayani Mbozi na stend kuu ya mabasi kutachochea ukuaji wa uchumi wa wilaya, mkoa na Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine amewahakikishia wananchi wa Kata ya Igamba kuhusu kujengwa kwa kituo cha afya ili kupunguza idadi ya vifo vya mama na mtoto ambavyo vimedaiwa kutokea kutokana na ukosefu wa huduma za afya.
Pia, Chongolo amewataka wananchi kushiriki katika ujenzi wa mradi wa shule ya kijiji cha Msanyila ambapo yeye amechangia mabati 150 ili kukamilisha ujenzi.