Spika Ndugai : Bungeni ni nyumbani, Uwaziri ni vyeo vya muda

0
178

Mawaziri na Naibu Mawaziri wametakiwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kutosahau kuwa wao ni Wabunge na uwaziri ni vyeo vya muda.

Kauli hiyo imetolewa bungeni jijini Dodoma na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, -Job Ndugai mara baada ya kuwaapisha Wabunge watatu walioteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan hapo jana.

Amesema ni vema Mawaziri na Naibu Mawaziri kufahamu bungeni ni nyumbani, na huko kwingine wanapokwenda ni matembezini, na endapo kitatokea chochote wanarudi nyumbani.

Spika Ndugai amewashauri Wabunge wanapoteuliwa kushika nyadhifa za Uwaziri ama Naibu Mawaziri kutolidharau Bunge na badala yake waendelee kushirikiana na Wabunge wenzao katika kutatua changamoto mbalimbali za Wananchi.

Amewataka Wabunge hao walioteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuapishwa hii leo, kwenda kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi hasa Liberata Mulamula ambaye pia ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mbarouk Nassoro Mbarouk aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mbunge mwingine aliyeapishwa hii leo ni Dkt. Bashiru Ally.