Spika Ndugai akabidhiwa hati ya jengo la Bunge

0
193

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amemkabidhi hati ya jengo la bunge Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Akipokea hati hiyo Spika Ndugai amesema kwamba sasa badala ya kuwa wapita njia na wapangaji, kwa hati hiyo anaamini wapo nyumbani.

“Nami nitoe wito kwa Taasisi zote za kiserikali wizara na mashirika kuhakikisha kwamba maeneo yao yote yamepimwa na yana hati,” amesema Spika Ndugai.

Lukuvi pia ametumia nafasi hiyo kuzitaka taasisi nyingine za Serikali kuhakikisha zinapima na kuchukua hati za maeneo wanayoyamiliki. Amesema upimaji huo unaweza kufanywa na wapima wa serikali au wapima binafsi ambao wamesajiliwa na Wizara ya Ardhi.

Kwa upande wa wananchi, Waziri Lukuvi amewataka wale ambao maeneo yao hayajarasimishwa wafanye hivyo kulinda milki zao na wale wanaomiliki kisheria wahakikishe wanalipa kodi zao kwa wakati kuepusha usumbufu utakaotokana na limbikizo la kodi hizo.

Amesisitiza kuwa wizara ya ardhi itaendelea kutoa ushirikiano kupitia ofisi zake zilizoanzishwa kila mkoa ili kurahisisha upimaji na upatikanaji wa hati kwa taasisi za serikali na jamii yote kwa ujumla.