Sokoine alikuwa mtumishi mwenye ujasiri

0
239

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amemtaja Waziri Mkuu wa zamani Hayati Edward Sokoine kama mtu aliyekuwa muadilifu na mchapakazi huku akiwataka Watanzania kumuenzi kwa kufanya kazi kwa bidii na kuwaenzi viongozi waadilifu na wachapakazi wa sasa wenye sifa za kufanana na za Hayati Sokoine.

Makonda ameyasema hayo wilayani Monduli alipotembelea makazi ya Hayati Sokoine eneo la Enguiki, kukagua maandalizi ya kumbukumbu ya miaka 40 ya kifo cha Sokoine, itakayofanyika kesho Aprili 12, 2024.

Makonda pia amesema Hayati Sokoine alikuwa mtumishi mahiri na mwenye ujasiri wa kusukuma gurudumu la maendeleo ya Watanzania bila kuogopa na kuhofia vikwazo.

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwaongoza Watanzania katika kumbukumbu hiyo hapo kesho.

Edward Moringe Sokoine alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania mara mbili. Kuanzia Februari 13, 1977 hadi Novemba 7, 1980, na Februari 24, 1983 hadi alipofariki dunia katika ajali ya gari Aprili 12, 1984.