Singida yaneemeka na tozo za miamala ya simu

0
224

Mkoa wa Singida umepokea mabilioni ya fedha kwa ajili ya kuendeleza elimu, miundombinu ya barabara, maji na afya ikiwa ni matokeo ya tozo za miamala ya simu.

Akizungumza na wananchi katika ripoti ya wiki ya Serikali, Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa amesema katika kipindi cha mwezi Septemba kiasi cha shilingi bilioni 2.27 zimeelekezwa katika ujenzi wa vituo nane vya afya mkoani humo ikiwemo katika wilaya ya Ikungi, Iramba, Itigi na Manyoni.

Msigwa amekumbusha lengo la ‘tozo za mshikamano’ ama tozo za miamala ya simu ni “kuharakisha utatuzi wa kero zinazowakabili Watanzania.”

Maeneo mengine yatakayonufaika kimaendeleo ni pamoja na vyumba vya madarasa 22 kujengwa kwa ajili ya kuanza kutumika Januari 2022, ujenzi wa barabara zinazoiunganisha Singida na mikoa ya jirani.

Ujenzi wa miundombinu ya maji safi na salama kwenye baadhi ya maeneo yenye shida ya maji ikiwemo Kintinku na Ibaga ni jambo ambalo Serikali haijaliacha nyuma kwa wakazi wa Singida.

Aidha, Serikali inaendelea kupanua wigo wa upatikanaji wa umeme mkoani huko ili kuweza kufikia vijiji vyote vya Singida. Hadi sasa vijiji 274 kati ya 441 vina umeme.