Msafara wa wachezaji 20 wa timu ya Simba ukiambatana na benchi la ufundi pamoja na baadhi ya viongozi umeondoka nchini asubuhiI Januari 17 kuelekea jijini Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kuwakabili As Club Vita katika mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Mchezo huo wa pili wa kundi De utachezwa jumamosi ya wiki hii January 19 majira ya saa moja jioni mjini Kinshasha na Kikosi cha SIMBA imesafiri bila ya nahodha wake John Bocco aliyemajeruhi ambapo nafasi yake imechukuliwa na Adam Salamba.
Katika mchezo wa kwanza wa kundi hilo, Simba ambao ndio vinara wa kundi, walianza vyema kwa kupata ushindi wa mabao matatu kwa bila dhidi ya Js Saoura ya Algeria katika mchezo uliochezwa Januari 12 katika uwanja wa Taifa jijini Dare es salaam.
Simba wanaongoza kundi lao la De wakiwa na alama tatu sawa na Al Ahly ya Misri, lakini Simba wana uwiano mzuri wa mabao ya kufunga ambapo wao wana mabao matatu huku Ahly wakiwa na mabao mawili.
Mchezo mwingine wa kundi hilo utachezwa kesho Ijumaa ambapo bingwa wa kihistoria wa michuano hiyo Al Ahly wanasafiri hadi nchini Algeria kumenyana na Js Saoura wanaoburuza mkia kwenye kundi lao.