Simamieni fidia kwa wafanyakazi wenu

0
307

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Dkt. John Mduma amesema kuna umuhimu kwa Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi kuhakikisha fidia stahiki inatolewa kwa wakati pindi wafanyakazi walio chini yao wanapoumia, kuugua au kufariki dunia wakati wakitekeleza majukumu yao nje ya nchi.

Dkt. Mduma ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi, wanaokutana kwenye Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere Kibaha mkoani Pwani.

Amesema WCF hutumia ofisi za Balozi za Tanzania nje ya nchi ili kuthibitisha uhalali wa madai ya mfanyakazi anayeumia, kuugua ama kufariki dunia wakati akitekelza majukumu ya mwajiri nje ya mipaka ya Tanzania, hivyo kuwataka Mabalozi hao kusimamia upatikanaji wa taarifa sahihi.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki January Makamba ametoa wito kwa Mabalozi hao hasa wale wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi za Zambia, Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambako kuna idadi kubwa ya madereva wa Kitanzania kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa kutosha kwa mfuko huo.