Siku 30 za shule kufungwa zikimalizika, makatibu wakuu wakutana Dodoma

0
1257

Wakati siku 30 za kufunguwa shule, vyuo vya kati na vyuo vikuu pamoja na taasisi nyingine za mafunzo zikielekea ukingoni, watu wengi wamekuwa wakijiuliza maswali endapo serikali itaruhusu wanafunzi kurejea kwenye taasisi zao za mafunzo au itaongeza siku za taasisi hizo kufungwa.

Wakati jambo hilo likigonga vichwa vya wananchi wengi hasa wazazi wenye wanafunzi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amewatoa hofu na kusema kwamba kamati ya kitaifa ya makatibu wakuu wa wizara zote inakutana leo jijini Dodoma na itatoa uamuzi juu ya jambo hilo.

“Najua kuna maswali, siku 30 zinakaribisha kwisha, lakini niwatoe wasiwasi Watanzania, kesho [ leo Aprili 4, 2020] tunakamati ya kitaifa ya makatibu wakuu inakutana hapa Dodoma. Tutajaribu kutathmini mambo yote ambayo tumeyachukulia hatua, na kuona tunakwenda vipi mbele,” amesema Dkt. Abbasi katika mahojiano na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Aidha, Abbasi ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali ameongeza kuwa baada ya kikao hicho huenda muelekeo mpya wa mapambano dhidi ya virusi vya corona ukatolewa.

Akizungumzia utofauti wa hatua zinazochukuliwa na nchi mbalimbali Dkt. Abbasi amesema “jamii za Kiafrika sio sawa na jamii za Ulaya, hivyo baadhi ya mbinu za kupambana na ugonjwa huu wa corona zinaweza kutofautiana baina ya nchi moja hadi nyingine, lakini mwisho wa siku kuna mambo ya msingi lazima yazingatiwe.”

Machi 17 mwaka huu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitangaza kufunga shule na vyuo vyote nchini ikiwa ni moja ya hatua nyingi zilizochukuliwa na serikali katika kuhakikisha inadhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Hatua nyingine ni pamoja na kuzuia shughuli za mikusanyiko ya watu, kuviagiza vyombo vya usafiri kutosimamisha abiria, kuwaweka karantini kwa siku 14 watu wote wanaoingia nchini, kuzuia safari za nje ya nchi kwa watumishi wa umma, na Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) kusitisha safari zote za kikanda na kimataifa.