Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa mafanikio yake makubwa tokea aingie madarakani ni kuleta umoja wa wananchi na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo wakati alipofanya mazungumzo na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya habari vya nje na ndani ya Zanzibar ikiwa ni siku 100 katika uongozi wake wa Serikali ya Awamu ya Nane, hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Zanzibar.
Akieleza kwa wananchi kupitia vyombo vya habari wakati akizungumza na waandishi hao, Rais Dk. Mwinyi aliyataja maeneo 10 ambayo ameyaeleza kwa ufupi ikiwa ni pamoja na kuwepo wa maridhiano na umoja wa Kitaifa.
Amesema kuwa wakati anaingia madarakani alitambua fika kwamba hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana bila ya kuwepo amani na umoja ndipo walipoanza mazungumzo kati yao na chama cha ACT-Wazalendo huku akisema kuwa bila ya kuwepo Serikali ya Umoja wa Kitaifa maendeleo yangekawia kwani mazingira yasingekuwa rafiki.
Amefafanua kwamba tayari ameunda serikali na amepunguza ukubwa wa serikali ili kupunguza gharama za utawala na badala yake fedha nyingi zielekezwe kwenye miundombinu na huduma za jamii sambamba na kuzingatia mambo yote katika uteuzi.
Kwa upande wa uchumi, amesema kuwa uchumi wa buluu ndio aliounadi wakati wa kampeni na tokea alipoingia madarakani ameweka mikakati maalum ya kuzungumza na wawekezaji na tayari mikataba ya awali imeshatiwa saini ikiwemo ujenzi wa bandari ya Mangapwani/Bumbwini ambayo itaifanya Mangapwani iwe mji wa Bandari.
Tayari Oman imeonesha nia ya mashirikiano huku akieleza jinsi utiwaji saini wa ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri ambayo utatekulezwa kwa dola za kimarekani bilioni 6.3 ambao ni mradi mkubwa sana huku bandari ya Malindi kugeuzwa kuwa bandari ya utalii.
Aidha, alisema hatua ya kuongeza uzalishaji wa umeme ambapo tayari Serikali imeshatiliana saini na Kampuni kutoka Marekani yenye kutaka kuzalisha umeme wa megawati 350 kwa awamu ili kuchochea uchumi wa Zanzibar.
Dkt. Mwinyi amesema hivi karibuni Serikali itakopa fedha kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kujenga miundombinu ya umeme wa jua pamoja na kuimarisha miundombinu itakayowezesha kupatikana kwa KV 135 ambayo itaweza kubeba umeme mkubwa.
Katika suala zima la miundombinu, amebainisha kuwa kwa kiwango kikubwa bandari ya Malindi imeweza kuimarika na kwenye mapato, imeweza kuingiza fedha nyingi ambapo kwa muda wa mwaka mmoja uliopita ilikuwa ikiingiza faida ya TZS bilioni 4.3 ambapo mwezi Disemba pekee imeweza kuingiza TZS bilioni 2.1 hatua ambayo imeonesha ufanisi mkubwa.
Aidha, ameeleza hatua za kuimarisha huduma za uwanja wa ndege wa Zanzibar sambamba na juhudi zinazochukuliwa katika kuhakikisha huduma katika kiwanja cha ndege cha Zanzibar zinaimarika.
“Hatua zilizochukulwia za awali kwamba hata wawekezaji kutoka nje wamevutika na wanataka kuja kuekeza Zanzibar sambamba na wale wawekezaji wa Zanzibar,” ameeleza.
Kwa upande wa wafanyabiasahra wadogo wadogo amesema hatua alizozichukua za kujenga maeneo na karibu soko lao la Kibandamaiti litafunguliwa karibuni.
Kuhusu sekta ya afya anesena serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuiimarisha ikiwa ni pamoja na kuanzisha kwa bima ya afya huku sekta ya elimu nayo ikiimarishwa.
Amesema suala la uwajibikaji limekuwa likipewa kipaumbe na hivi sasa na kazi zimeanza kufanyika na kutoa mfano kwa Mashirika ya ZECO, Mamlaka ya ZAWA, Wakala wa Barabara nao wamekuwa wakitekeleza vyema kazi zao huku juhudi za makusudi zikiendelea katika kutatua migogoro ya ardhi.
“Serikali haitaki masihara katika masuala ya rushwa na tumechukua hatua kila kasoro na tutaendelea kufanya hivyo na hiyo sio nguvu za soda na hatua zitaendele kuchukuliwa.”
Ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ni jambo jingine alilogusia ambapo amesema katika kipindi hichi cha siku 100, mapato ya kodi yameongezeka sana na kusema kuwa bado hajaridhika na ukusanyaji huo huku akieleza kwamba Serikali inajipanga kufunga mifumo ya kielektroniki katika maeneo yote hatua ambayo itaongeza pato la serikali.
Kwa upande wa suala la udhalilishaji amesema kuwa vituo vya uchunguzi vifanye kazi ya ziada na kwa upande wa Mkurugenzi wa Mashtaka kesi ziende kwa haraka ambapo pia tayari mahakama maalum ya udhalilishaji imeshaanzishwa na kusisitiza kwamba hivi karibuni katika kikao cha Baraza la Wawakilishi ameagiza Serikali ipeleke maelekezo ili kesi za udhalilishaji zisiwe na dhamana.
Kuhusu ushirikiano na sekta binafsi, amefafanua kuwa hatua kubwa zimechukuliwa na sekta hiyo tayari kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Nane kutokana na mwitikio mkubwa sana zikiwemo benki na kuahidi kuimarisha mazingira ya biashara visiwani Zanzibar.
Amesema kuwa siku 100 za kwanza za Serikali ya Awamu ya Nane zimethibitishwa kwamba serikali iko makini na imekusudia kutekeleza ahadi ilizozitoa kwa wananchi imezingatia misingi iliyowekwa na Serikali zilizopita, na kutoa shukrani kwa wasaidizi wake wakuu kwa kumsaidi majukumu yake na kuwashukuru viongozi wa umma kwa kutekeleza vyema majukumu yao.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa Serikali imejipanga kujenga mifumo ya kielektroniki hatua za makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha suala la ajira linaondokana na changamoto iliyopo.