SIDO yaagizwa kujenga kituo cha teknolojia ya kuongeza uzalishaji

0
207

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaudi Kigahe ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) kujenga kituo kikubwa cha kuendeleza teknolojia katika mkoa wa Dodoma chenye uwezo wa kutengeneza bidhaa mbalimbali za mashine kulingana na soko la ushindani.

Kigahe ameyasema hayo alipokuwa akiongea na menejimenti na wafanyakazi wa Ofisi ya SIDO mkoa wa Dodoma alipokuwa katika ziara ya kukagua miradi inayosimamiwa na SIDO, mitaa ya viwanda na wajasiliamari wanaowezeshwa na SIDO.

Wajasiriamali waliotembelewa walieleza changamoto mbalimbali kama vile upatikanaji wa vifungashio haswa vya mvinyo kwa kuwa vifungashio vingi vinaagizwa kutoka nje ya nchi, upatikanaji mdogo wa mitaji ya kuendeleza biashara kwa kuwa Mfuko wa NEDF hauna mtaji wakutosha na kima cha juu cha kukopa ni kidogo kulingana na mahitaji ya viwanda na upatikanaji wa malighafi ya uzalishaji hususani wa mvinyo ambazo hazipatikani kwa mwaka mzima na kufanya viwanda hivyo kutokuzalishwa mvinyo kwa mwaka mzima.

Mkurugenzi wa SIDO, Mhandisi Prof. Sylvester Mpanduji amesema SIDO imeendelea kutekeleza majukumu kwa kutoa huduma za kiufundi na maendeleo ya teknolojia, uanzishaji wa miradi ya viwanda vidogo vijijini, mafunzo, ushauri na huduma za ugani, masoko na habari, na huduma za fedha kwa wajasiliamali wadogo ili kuendeleza sekta ya viwanda na biashara na kuchangia katika ukuaji wa uchumi.