Shule yafungwa baada ya tukio la tatu la moto

0
364

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule ameifunga Shule ya Sekondari ya Wavulana Geita (GESECO) kwa muda wa wiki mbili baada ya moto kuwaka katika bweni la wavulana usiku wa kuamkia leo Julai 14, 2021.

Kutokana na uamuzi huo, wanafunzi wote wametakiwa kurudi majumbani, na wanafunzi wanaosoma kidato cha tano watahamishiwa katika shule zingine za sekondari zilizopo katika mkoa huo.

Kufuatia tukio hilo, wanafunzi watatu wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita baada na kupata matatizo ya kiafya, ambapo vifaa vyao yakiwemo magodoro, masanduku na nguo na mali nyingine za shule vimeteketea.

Hii ni mara ya tatu kwa shule hiyo kuungua moto ndani ya kipindi kifupi cha wiki mbili ambapo awali darasa lililokuwa likitumiwa kuhifadhi magodoro na masanduku ya wanafunzi liliungua, kisha ikifuatiwa na kuungua kwa maabara ya kemia na baiolojia na kupelekea kuharibika kwa mali mbalimbali.