Mkutano wa tisa wa Bunge la 12 umeanza leo jijini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine wabunge watakuwa na kazi ya kupokea na kujadili taarifa za kazi na majukumu ya kamati za kudumu za bunge kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022, ambazo zilianza kukutana Oktoba 9 hadi Oktoba 28 mwaka huu.
Pia Wabunge watatumia majuma mawili ya mkutano huo kujadili na kupitisha miswada ya sheria ambayo ilisomwa kwa mara ya kwanza bungeni katika mkutano wa nane wa bunge la 12.
Miswada hiyo ni pamoja na Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambao kama bunge litaupitisha utekelezaji wake utaanza mwaka ujao wa fedha.
Pia wabunge wanatarajiwa kupitisha Muswada wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali na Muswada wa Sheria ya Uwekezaji Tanzania.
Tayari Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imepokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali katika miswada hiyo.