Shisha kwa saa moja sawa na sigara 100

0
228

Kamishna Msaidizi wa Kinga na Huduma kwa Jamii wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini (DCEA), Moza Makumbuli amesema kuwa kitendo cha mtu kuvuta shisha kwa saa moja ni sawa na kuvuta kati ya sigara 100 hadi 200, pia ameongeza kuwa wapo baadhi ya wafanyabiashara wenye nia ovu zaidi huongeza baadhi ya dawa za kulevya ikiwamo bangi na Cocaine.

Ametoa ufafanuzi huo leo alipokuwa akiwasilisha mada katika kikao kazi cha Waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya kidigitali (Online Media) kinachofanyika Morogoro kuanzia leo Novemba 10 hadi 12, 2021.

“Uhalifu wa dawa za kulevya upo mitaani, shisha ni utamaduni uliokuja nchini mwetu, lakini tofauti na wenye utamaduni wao ambao kiuhalisia kifaa hicho walikuwa wanakitumia kifaa hicho kuvuta tumbaku, lakini kwetu sisi zinaongezwa ladha mbalimbali na hata kuwekwa dawa za kulevya,” amesema Moza Makumbuli.

Awali, mmoja wa waandishi wa habari aliuliza swali kuhusu DCEA inachukua hatua gani kwani hivi sasa kunaonekana wazi kuwapo wimbi la matumizi ya shisha kwenye kumbi nyingi za starehe, ikikumbukwa kwamba siku za awali iliwekeza nguvu kubwa kudhibiti matumizi ya bidhaa hizo.

Akijibu swali hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa DCEA, Florence Khambi amesema Mamlaka imepokea hilo kama taarifa na watalifanyia kazi kasha watatoa taarifa ya kina kwa jamii.

Aidha, Florence Kambi Ameongeza kuwa “Ieleweke kuwa udhibiti wa matumizi ya tumbaku na bidhaa za tumbaku hayapo chini yetu kwa sheria na kanuni, bali tunashirikiana kwa ukaribu na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ndipo tuweze kuchukua hatua zaidi”.