Shigela : Watumishi waadilifu nao ni mashujaa

0
207

Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigela amesema Watumishi wanaofanya kazi kwa uadilifu, weledi, kujitolea pamoja na kujibidiisha kwa ajili ya ujenzi wa Taifa lao nao pia ni Mashujaa.

Shigela amesema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa yaliyofanyika kimkoa katika uwanja wa Mashujaa Mjini Geita.

“Tumeshuhudia Madaktari wanavyofanya kazi majira ya usiku kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu.. hao ni mashujaa, walimu pia tumeona namna wanavyopambana kuwafundisha watoto wetu na hata siku zingine wanajitolea siku za mapumziko hao pia ni Mashujaa,” Amesema Shigela

Aidha, ameiagiza halmashauri ya Mji Geita kuutunza uwanja huo Mashujaa kwa kufanya usafi na ukarabati na endapo watashindwa kufanya hivyo waukabidhi kwa Jeshi la Magereza mkoani Geita ili wautunze.

Wakati wa maadhimisho hayo ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa kimkoa mkoani Geita, washiriki wamefanya usafi pamoja na kupanda miti katika uwanja huo wa Maashujaa.