Shaka Ssali astaafu utangazaji

0
170

Mtangazaji mkongwe raia wa Uganda wa Kipindi cha Straight Talk Africa kinachorushwa na kituo cha runinga na redio cha Sauti ya Amerika cha nchini Marekani (VOA) Shaka Ssali, amestaafu rasmi majukumu yake ya uandishi wa habari na utangazaji.

Taarifa iliyotolewa na uongozi wa VOA, Shaka Ssali amestaafu baada ya kukitumikia kituo hicho kwa kipindi cha miaka 29, ambapo mbali na Straight Talk Africa, alikuwa pia akitangaza kipindi kingine cha Shaka: Extra Time.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba Shaka ataongoza kipindi cha mwisho cha Straight Talk Africa Jumatano ya Mei 19, 2021 ambacho kitakuwa maalum kwa ajili ya kumuaga na kuonesha heshima kwa mchango mkubwa alioutoa kwa kipindi chote alichokuwa akifanya kazi na VOA.

Kipindi cha mwisho cha Shaka, kitakuwa ni maalum kwa ajili ya kuangazia safari ya uandishi wa habari ya mwanahabari huyo nguli kuanzia mwanzo alipojiunga na kituo hicho na jinsi alivyoitumia taaluma yake kuboresha demokrasia na maendeleo kwa nchi za Afrika.

Taarifa hiyo ya VOA imeongeza kwamba siku hiyo ndipo atakapotambulishwa mrithi wa Ssali katika kipindi hicho cha Straight Talk Africa.