Shaka atoa maagizo changamoto za shule mkoani Mtwara

0
191

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka amewataka watendaji wa halmashauri za wilaya na mikoa kutanguliza utu na ubinadamu katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi.

Shaka amesema hayo baada ya kutembelea Shule ya Sekondari Chidya iliyopo wilayani Masasi mkoani Mtwara ambayo pia ina wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Akiwa shuleni hapo alikuta changamoto mbalimbali ikiwemo ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata maji ambayo hata hivyo imedaiwa sio salama, ubovu wa barabara, kukosekana kwa daktari wa shule na kutokuwa na gari kwa muda mrefu baada ya lililokuwepo kuharibika.

Kuhusu malalamiko ya wanafunzi kuhusiana na maji, Shaka amesema anazo taarifa kwamba mbali na kuyafuata umbali mrefu, pia kuna malalamiko ya wanafunzi wengi kusumbuliwa na matumbo ya kuhara, hivyo ameagiza hatua za haraka zichukuliwe kwa kupeleka dawa za kusafisha maji ili kunusuru afya za wanafunzi hao ambazo ziko hatarini .

Kwa upande wa changamoto ya miundombinu ya barabara Shaka alitoa maelekezo kwa serikali ya Mkoa wa Mtwara kupitia Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) kuhakisha inaifanyia matengenezo barabara inayokwenda shuleni hapo ili kuwasaidia wanafunzi na wananchi kwa ujumla.

“Nimelazimika kusimama hapa kwa sababu nimepewa salamu zenu na Rais Samia Suluhu Hassan, anawasalimieni sana. Anafahamu kwamba kuna Chidya na wito wake, endeleeni kufanya vizuri. Anatumia fedha nyingi sana kuwekeza kwenye elimu ikiwemo ujenzi wa madarasa.”

Akizungumza katika ziara hiyo, mkuu wa Mkoa huo Brigadier Jenerali Marko Gaguti, alisema amepokea maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatafanyiwa kazi kwa haraka.

Kuhusu suala la maji kutokuwa salama kwa wanafunzi wa Chidya mkuu huyo wa mkoa ameahidi leo watapelekewa mifuko mitano ya dawa ya kusafisha maji.