Inspekta Innocent Ndowo ambaye ni shahidi wa 10 katika kesi ya Uhujumu Uchumi yenye mashitaka ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watatu ameshindwa kumaliza kutoa ushahidi wake mahakamani baada ya kuugua ghafla.
Ndowo ambaye ni Inspekta wa Polisi katika kitengo cha Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi katika masuala ya kimtandao ameshindwa kukamilisha kutoa ushahidi wake baada ya kupata tatizo la kiafya.
Awali kabla ya kupata tatizo hilo Ndowo ameiambia kuwa yeye kama mtaalamu mwenye ujuzi wa kompyuta na simu za mkononi kwenye kitengo hicho, ana jukumu la kupokea vielelezo mbalimbali vinavyohusishwa na makosa ya kimtandao kisha kuvifanyia uchunguzi kulingana na maombi ya taasisi husika inayofanya upelelezi juu ya makosa ya kimtandao.
Amesema uchunguzi wa vifaa vya kielekroniki ambavyo ni vielelezo unazingatia hatua tatu ikiwa ni pamoja na kufanya uchambuzi wa vielezo husika kwa kutumia vifaa maalumu vya maabara.
Aidha ameeleza kuwa Julai Mosi mwaka 2021 Ofisi ya DCI ilimwomba afanye uchunguzi wa miamala ya fedha na mawasiliano simu kwenye laini za simu za mtandao wa Airtel na Tigo pamoja na simu nne na kwamba baada ya uchunguzi alibaini laini hizo zilisajiliwa kwa majina ya Freeman Mbowe, Halfan Bwire na Denis Urio.
Ameeleza zaid kuwa baada ya kuandika ripoti juu ya uchunguzi wa vilelezo hivyo ikiwemo barua kutoka Kampuni ya Tigo na Airtel alivikabidhi vielelezo hivyo na ripoti kwa Afande Swila kwa ajili ya hatua nyingine za kiupelelezi.
Hata hivyo upande wa jamhuri unaoongozwa na Wakili Robert Kidando umeomba kuahirishwa kwa shauri hilo hadi Januari 18 baada ya shahidi huyo kupata tatizo la kiafya wakati akiendelea kuhojiwa na Wakili wa Serikali Pius Hila.
Upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala umesema hawana pingamizi juu ya ombi hilo huku wakiomba mahakama kuangalia uwezekano wa kuendelea na shahidi mwingine iwapo shahidi huyo wa 10 atashindwa kurejea kwenye hali yake ya kawaida kwa wakati muafaka.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 18 kwa ajili ya mahakama kuendelea kusikiliza ushahidi kwa upande wa jamhuri na washitakiwa wamerudishwa rumande.