Na,Emmanuel Samwel,Dar es Salaam.
Shahidi namba moja katika shauri dogo ndani ya kesi kubwa ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe na wenzake watatu ameendelea kutoa ushahidi wake.
Utaratibu uliowekwa na askari wa usalama katika eneo la Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi iliyopo mkoani Dar es Salaam ni watu wachache kuingia ndani ya chumba cha mahakama kuwakilisha makundi yao wakiwemo Waandishi wa habari 10 Mawakili 20, Wanafamilia 5, wageni maalum 3 na Viongozi wa CHADEMA 5.
Utaratibu huo mpya ambao haujazoeleka katika mahakama nchini, umesabisha mvutano mkali kati ya Mawakili wa upande wa utetezi pamoja na wale wa Jamhuri, ambapo Mawakili wa utetezi waliona ni vema kesi hiyo iahirishwe kuliko watu wazuiliwe kuingia ndani ya mahakama.
Utaratibu huo pia uliyataka makundi yote isipokuwa Mawakili na Wanahabari kutoingia na simu za mkononi.
Baada ya saa tatu za mvutano, mahakama hiyo iliamuru watu wote kuingia katika chumba cha mahakama bila simu, hali iliyosabisha watu wote kutolewa kwa ajili ya ukaguzi.
Hata hivyo malumbano yaliendelea mpaka Jaji anayeendesha shauri hilo aliporuhusu watu kuingia na simu kwenye chumba cha mahakama ili kesi iweze kuanza.
Baada ya utaratibu kuwekwa sawa, kesi ilianza majira ya saa saba mchana ambapo shahidi namba moja ambaye ni Kamanda wa polisi wa mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni Ramadhani Kingai katika shauri dogo akaanza kutoa ushahidi wake akiwa anaongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Robert Kidando mbele ya Jaji Mustapha Siyani.
Akiongozwa kujibu maswali na wakili Kidando, shahidi huyo ameieleza mahakama kuwa daftari la kutunzia taarifa (Note Book) ambayo ilitakiwa kuwa kielelezo cha ushahidi katika kesi hiyo halikuwa na ulazima wa kupeleka mahakamani kwa madai linatumika kutunza kumbukumbu mbalimbali ambazo zingine ni za siri.
Wakili wa Serikali: akamuuliza shahidi pia kuhusu mtuhumiwa kukutwa akiwa na silaha na hukumuonya kwa kosa hilo, ndipo shahidi huyo akasema hakufanya hivyo kwa madai kuwa alimuonya mtuhumiwa kwa kesi kubwa ya kula njama za kutenda matendo ya kigaidi na kwamba hayo mengine yangeingia ndani ya kesi hiyo.
Baada ya shahidi huyo kutoa ushahidi wake mbele ya mahakama hiyo, wakili Mwandamizi wa Serikali Robert Kidando akaomba kuahirishwa kwa kesi hiyo kutokana na shahidi namba mbili kutofika mahakamani na kwamba yuko nje ya mkoa wa Dar es Salaam.
Hata hivyo Jaji Mustapha Siyani ameahirisha kesi hiyo hadi tarehe 17 mwezi huu ambapo upande wa Jamhuri utaendelea kutoa ushahidi wake.
Katika hatua nyingine Magdalena Ntandu ambaye ni Msajili wa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ametolea ufafanuzi mvutano uliotokea mahakamani hapo kati ya Mawakili wa pande zote mbili kuhusu watu kuingia ndani chumba cha mahakamani wakiwa na simu za mkononi na kusababisha kuchelewa kuanza kwa kesi na kusema kuwa utaratibu huo unalenga kuzuia usambazaji wa taarifa za upotoshaji mtandaoni wakati kesi inaendelea.