Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby amesema kuwa wapigaji wa fedha za umma wamekuwa wengi, na wamejikita kwenye kusifia kuwa ‘Mama Anaupiga Mwingi,’ lakini kiuhalisia wao ndio wanaoupiga mwingi kwa kuiba fedha za umma.
Amesema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akichangia Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/25 na kuongeza kuwa utaratibu wa kuacha taasisi kukusanya fedha unachochea vitendo vya wizi wa fedha za umma.
Shabiby amepinga mpango wa Serikali kuziacha taasisi kukusanya fedha, badala yake utaratibu uliokuwa unatumika na Serikali ya awamu ya tano wa fedha zote kwenda Serikali kuu, kisha taasisi hizo ziombe na kupewa kwa mujibu wa bajeti zao, ndio utumike.
“Mimi nafikiri ule mpango wa awamu ya tano haukuwa mbaya; wa kuchukua fedha zote halafu wao [taasisi] waandike bajeti […] ninyi msiwacheleweshee tu kuwapelekea, halafu zinazobaki kwa mwaka ndio gawio,” amesema Shabiby na kueleza kushangwazwa na watu wanaosifia taasisi zinazokusanya fedha nyingi zikitoa gawio dogo serikalini.
Amesema kuwa Waziri wa Fedha anatakiwa kuwa ngangari na kwamba akitaka kuwa mzuri kwa kila taasisi ikusanye fedha zake, kazi yake itakuwa ngumu na kama ameshindwa, ampishe hata yeye akalie kiti hicho.
“Nchi imefikia wakati sasa hivi, lazima tuseme ukweli, wapigaji wamekuwa wengi. Wengine utasikia tu, ‘Mama Anaupiga Mwingi,’ sio kwamba anaupiga mwingi anamsifia kwenye moyo, anaupiga mwingi yeye anaiba hela,” ameeleza.
Katika hatua nyingine amehoji Serikali kushindwa kutekeleza ahadi yake ya kukopesha magari kwa watumishi wa umma wanaostahili kupewa magari, badala ya Serikali kubeba mzigo wa kuwanunulia ni kugharamia magari kama njia ya kupunguza matumizi ya Serikali.
Pia, ameishauri Serikali kupiga mnada magari mabovu yaliyoko kwenye halmashauri ili kukusanya fedha, kama moja ya vyanzo vya mapato.