Rais Samia Suluhu Hassan leo amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa, mazungumzo ambayo yamehusu maendeleo ya miradi ya ujenzi wa reli na maendeleo ya shirika hilo.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam, Kadogosa ameishukuru Serikali kwa kuidhinisha shilingi Bilioni 372.34 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kipande cha tano cha reli ya Mwanza – Isaka chenye urefu wa kilometa 341 kwa kiwango cha kisasa.
Amesema ujenzi wa reli katika vipande viwili unaendelea vizuri ambapo hadi mwezi Aprili mwaka huu kipande cha Dar es salaam hadi Morogoro chenye urefu wa kilomita 300 kilikuwa kimefikia asilimia 91 na kile cha Morogoro hadi Makutupora chenye urefu wa kilomita 422 kilikuwa kimefikia asilimia 60.02.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa TRC amemueleza Rais Samia Suluhu Hassan kuwa, majaribo ya treni ya abiria yanatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu kwa kipande cha Dar es salaam hadi Morogoro.
Kwa upande wake Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha ujenzi wa reli ya kati utakaounganisha bandari ya Dar es salaam na mikoa ya kanda ya ziwa na kanda ya magharibi unakamilishwa ili kuzifikia nchi za Uganda, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Amemuagiza Kadogosa kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo ya ujenzi vizuri ikiwa ni pamoja na kujipanga kwa ajili ya ujenzi wa vipande vya Makutopora – Tabora, Tabora – Isaka na Kaliua – Mpanda – Kalema.
Rais Samia Suluhu Hassan ameipongeza TRC chini ya Kadogosa pamoja na wote wanaoshiriki katika ujenzi wa reli kwa kazi nzuri wanayoifanya, na ameeleza kuridhishwa na maendeleo ya miradi hiyo.