Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas amezindua kituo cha Dar es Salaam cha Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya.
Chuo cha maendeleo ya Michezo Malya, ni Chuo pekee kinachotoa stashahada ya michezo hapa nchini kwa kuzingatia mitaala ambayo imepitishwa na wataalam kutoka vyuo vikuu vya kimataifa. Chuo hiki kinatoa Stashahada ya Utawala na Uongozi katika Michezo, Stashahada ya Elimu ya Michezo na Stashahada ya Ukocha.
Pamoja na uzinduzi wa chuo hicho, Dkt Abbas ameshuhudia uwekaji saini wa Mkataba wa makubaliano kati ya chuo cha Malya na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)ili kufanya kazi kwa pamoja na kuweza kutoa wataalamu wa michezo nchini.
“Mkataba uliosainiwa leo ni kati ya Malya na TFF hivyo ninaomba mikataba mingine mingi ifuate kutoka kwa mashirikisho mengine ya michezo nchini. Na natoa siku 60 kwa kila shirikisho linaloona kwenye kile wanachokisimamia kuna kitu wanaweza kushirikiana na chuo cha Malya wawe wamesaini mkataba” amesema Dkt Abbas.
Dkt Abbas ameongeza kuwa agizo hilo ni kwa chuo chenyewe na kumtaka Mkuu wa Chuo akutane na marais na wenye viti ambao wakiingia nao mkataba watasaidia michezo itoke kwenye maneno na kwenda kwenye utendaji hivyo kukuza sekta ya michezo nchini.