Serikali yazimwagia sifa timu za Taifa kwa ushindi

0
611

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi kwa niaba ya Serikali amewapongeza wanamichezo mbalimbali waliofanya vizuri katika uga mbalimbali wa michezo hivi karibuni.

Pongezi za kwanza ni kwa Timu ya Taifa ya Wanawake Chini ya Miaka 17 kwa kutwaa ubingwa wa kombe la COSAFA baada ya kushinda kwa penalti 4-3 dhidi ya Timu ya Taifa ya Zambia katika fainali zilizomalizika leo nchini Afrika Kusini.

Aidha, Dkt. Abbasi ametoa kongole kwa bondia Hassan Mwakinyo kwa kutetea mkanda wa Chama cha Kimataifa cha Ndondi (WBF) dhidi ya Muargentina, Carlos Paz hapo Jana Jijini Dar es Salaam.

Vilevile ameipongeza Timu ya Taifa ya Vijana Chini ya Miaka 17, Serengeti Boys, ambayo leo imeifunga 1-0 Timu ya Taifa ya Morocco Chini ya Miaka 17 jijini Rabat Morocco, katika mchezo mkali wa kirafiki ikiwa ni matayarisho ya Kufuzu Fainali za Afrika kwa Vijana.

“Serikali na Watanzania wote tunajivunia mafanikio haya na kama ambavyo Rais ameagiza, katika miaka hii mitano tutawekeza zaidi katika michezo kwa sababu eneo hili ni nguvu nyingine ya muhimu na ya kimkakati ya Taifa letu,” amesema Dkt. Abbasi.
Katika salaam hizo pia amewatakia kila kheri Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ambayo licha ya jana kufungwa kwa taabu 1-0 na Tunisia ugenini bado ina nafasi ya kufanya vyema zaidi katika mechi zijazo.