Serikali yaweka matumaini kwa Stars

0
168

Serikali imesema uwezekano wa timu ya Taifa ya Soka (Taifa Stars) kufanya vizuri katika michezo ya kuwania kufuzu fainali za kombe la FIFA la dunia zitakayofanyika nchini Qatar mwaka 2022 ni mkubwa, kutokana na matokeo mazuri ambayo imeyapata katika michezo minne ya awali.
 
Kauli hiyo imetolewa mkoani Dodoma na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa kikao na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa, uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na wadau wa mpira wa miguu.
 
 “Tukifanikiwa kushinda mechi hizo mbili zilizobaki kati ya timu ya Taifa na Congo pamoja na mechi ya timu ya Taifa na Madagascar ambayo itachezwa ugenini, itatupa matumaini ya kushiriki katika michuano ya kombe la dunia, hivyo Serikali inaamini ushirikiano kati ya wadau na uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni muhimu katika kufanikisha lengo hilo.” amesema Waziri Mkuu Majaliwa
 
Amesema michuano ya kombe la dunia ni fursa kwa wachezaji wa Tanzania, kwani itawasaidia kutambulika katika mataifa mbalimbali duniani pamoja na kupata nafasi ya kuhitajika na vilabu vikubwa duniani.
 
 Waziri Mkuu Majaliwa amewaeleza wadau hao wa mpira wa miguu nchini kuwa, Rais Samia Suluhu Hassan anatamani kuona Taifa Stars inafanya vizuri kama ilivyo kwa timu ya Taifa ya soka ya Wanawake ambayo hivi karibuni ilichukuwa ubingwa kwenye mashindano ya kombe la COSAFA 2021 yaliyofanyika nchini Afrika Kusini.