Serikali yawatoa hofu wananchi kuhusu Ebola

0
184

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amewatoa hofu Watanzania kuhusu ugonjwa wa Ebola uliopo nchi jirani, na kuwataka waendelee kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo.

Waziri Ummy ameyasema hayo mkoani Kagera, wakati wa ziara yake ya kukagua utayari wa mkoa huo katika kukabiliana na ugonjwa wa Ebola.

“Tunatakiwa kuongeza jitihada za kuzuia ugonjwa huo usiingie hapa nchini, niwakumbushe wananchi kuendelea kuchukua tahadhari zote tunazoelekezwa na wataalamu wa afya kama vile kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kutokugusana mikono na uonapo dalili nenda kituo cha kutolea huduma za afya.” ameelekeza Waziri Ummy Mwalimu

Naye, mkuu wa mkoa wa Kagera, Albert Chalamila amemeiomba serikali kujenga kituo maalumu mkoani humo cha kutenga wahisiwa wa magonjwa ya mlipuko (Isolation Center)katika mpaka wa Mulongo pamoja na wilaya ya Ngara – mpaka wa Rusumo, Murusagamba na Kabanga.

Chalamila pia ameishukuru wizara ya Afya kwa kuipatia hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kagera kipimbo cha CT – Scan pamoja na vifaa tiba vingine ambavyo tayari vimeanza kusimikwa.