Serikali imeahidi kuendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha inawalinda raia na mali zao, ili waweze kuendesha shughuli zao kwa amani na utulivu.
Ahadi hiyo ya Serikali imetolewa Bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa ahadi hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa jimbo la Makete lililopo mkoani Njombe, – Festo Sanga aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali katika kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyoendelea katika maeneo mbalimbali nchini ukiwemo ujambazi.
“Hata Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kupitia hotuba yake moja ya kitaifa amewaonya wote wanaofikiria huu ni wakati wa kufanya maovu nchini na amewataka wote wanaofikiria kufanya hivyo waache mara moja, haya pia ni maagizo kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua wote wanaosababisha madhara ya usalama kwa Watanzania,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Ametoa wito kwa Watanzania kushiriki katika suala la ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa kila wanapoona kuna dalili za uvunjifu wa amani katika maeneo yao, ili vyombo vya ulinzi na usalama viweze kuchukua hatua.