Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali haikubaliani na hali ya utoaji wa adhabu kwa wanafunzi, ambazo wakati mwingine zinakuwa kali na haziendani na miongozo ya utoaji adhabu hizo kwa wanafunzi.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema adhabu hizo si tu hazikubaliki bali zinatengeza msongo wa mawazo kwa wanafunzi na kuharibu afya na saikolojia ya watoto.
Amesema matukio ya adhabu kwa watoto yanazusha taharuki kwa jamii, lakini kwa masikitiko makubwa adhabu hizo zinatolewa na walimu wenye mafunzo na wakati mwingine wanaotoa adhabu hizo ni walimu wakuu.
Waziri Mkuu amesema waraka namba 24 wa mwaka 2002 wa wizara ya Elimu unatoa maelekezo ya adhabu ya viboko kwa wanafunzi ambapo adhabu ya juu inapaswa kuwa viboko 4 na mwanafunzi wa kike anapaswa kuchapwa mkononi na mwalimu wa kike.
Amewataka walimu na walezi kuzingatia miongozo ya sheria ya mtoto ya mwaka 2009 inayoeleza namna ya kuwalea watoto na adhabu zinazopaswa kutolewa kwa watoto.
Akichangia taarifa hiyo ya Waziri Mkuu, Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson amesema watoa taarifa wa matukio hayo ya ukatili kwa wanafunzi walindwe na wasichukuliwe hatua ili jamii iendelee kupata taarifa hizo na kuchukua hatua kwa wahusika.
Waziri Mkuu ametumia kanuni ya 44 Ibara ya 4 ya Bunge inayompa nafasi kutumia kipindi cha maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu kutoa taarifa ama ufafanuzi kwa jambo lolote lenye maslahi kwa Taifa.