Serikali imewapongeza wasanii watatu wa Bongo Fleva ambao wameshinda tuzo mashuhuri za muziki duniani AFRIMMA zilizotangazwa jijini Dalas nchini Marekani.
Wasanii walioibuka kidedea katika tuzo hizo ni pamoja na Naseeb Abdul maarufu Diamond Platinumz ambaye ameshinda kipengele cha Mwanamuziki Bora wa Kiume Afrika ya Mashariki, Faustina Mfinanga maarufu Nandy ambaye ameshinda kipengele cha Mwanamuziki Bora wa Kike Afrika Mashariki na Zuhura Othman maarufu Zuchu ambaye ameshinda kipengele cha Mwanamuziki Bora Anayechipukia Afrika.
Akitoa pongezi hizo kwa niaba ya Serikali Katibu Mkuu wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt.Hassan Abassi amesema tuzo hizo ni ishara wazi kwamba nchi imejaliwa kuwa na vipaji vingi vya thamani katika uwanda wa kizazi kipya.
“Serikali kama alivyoahidi Rais katika hotuba zake, itaendelea kuwawekea mazingira bora wasanii wetu katika miaka hii mitano ili kuongeza ufanisi zaidi ya haya,” amesema Abassi.
Tuzo za AFRIMMA hutolewa kila mwaka ikiwa ni ushirikiano kati ya Taasisi ya AFRIMMA ya nchini Marekani na Umoja wa Afrika (AU) ili kuenzi kazi, vipaji na ubunifu wa wasanii barani Afrika.