Serikali yatangaza kuvigawa Viwanda vilivyobinafsishwa na kurudishwa

0
176

Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo ametangaza fursa za uwekezaji katika Viwanda 20 vilivyokuwa vimebinafsishwa na kurejeshwa Serikalini

Waziri Mkumbo ameyasema hayo wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu fursa za kuwekeza katika Viwanda vilivyobinafsishwa na kurejeshwa Serikalini leo tarehe 23 Agosti 2021 katika ukumbi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) jijini Dar es salaam.

Akiongea na Waandishi hao, Prof. Mkumbo amefafanua kuwa Serikali ilifanya tathimini mwaka 2017 katika Viwanda 156 vilivyobinafsishwa tangu mwaka 1990 na kubaini kuwa Viwanda 88 vinafanya kazi kwa kuzingatia matakwa ya mikataba husika na Viwanda 68 vilikuwa havifanyi kazi kwa mujibu wa mikataba husika

Profesa Mkumbo amesema Serikali ipo katika hatua ya kurudisha Viwanda 48 kati ya Viwanda 68 visivyofanya kazi kwa mujibu wa mikataba husika kwa hatua zingine za uwekezaji ambapo hadi sasa Viwanda 20 havina mgogoro wa kisheria na viko katika hatua ya uwekezaji.

Viwanda 10 vitakavyokabidhiwa kwa Sekta Binafsi kwa ajili ya uwekezaji ni pamoja na Kiwanda cha Kilimanjaro Paddy Hauling kilichopo Kilimanjaro, Polysacks Company Ltd kilichopo Dar es salaam, NMC Isaka Rice Mill Company Limited kilichopo Shinyanga na Multpurpose Oil seed Processing Co.ltd (MOPROCO).

Viwanda vingine ni pamoja na CDA Intergrated Concrete Industry Kilichopo Dodoma, Manawa Generies Ltd kilichopo Mwanza, NMC Tabora Rice Mill kilichopo Tabora, Musoma Textikes Mills kilichopo Musoma, NMC Mzizima Maize Mill kilichopo Dar es salaam na Pesticides Manufacturers limited – Moshi kilichopo Kilimanjaro .

Viwanda nane (8) vinavyokabidhiwa kwa EPZA ni pamoja na Mwanza Tanneries kilichopo Mwanza, TPL Shinyanga Meat Plant kilichopo Shinyanga, Mafuta Ilulu kilichopo Lindi, Nachingwea Cashewnut kilichopo Lindi, TPL Mbeya kilichopo Mbeya, Sikh Sawmill Limited kilichopo Tanga na National Steel Corporation kilichopo Dar es salaam.

Prof Mkumbo pia alibainisha Viwanda viwili (2) vitakavyokabidhiwa Mashirika ya Umma ni pamoja na Mag’ula Mechanical MachineTolls kilichopo Mororgoro kitakabidhiwa kwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Mbeya Ceramics Co. Ltd kitakabidhiwa kwa Shirika la Kuhudumia Viwanda vidogo (SIDO).

Aidha amesema Wawekezaji wenye nia na uwezo wa kuwekeeza katika Viwanda hivyo wawasilishe maombi yao Ofisi ya Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara ambapo zoezi la kuwapata wawekezaji litafanyika kwa uwazi na ushindani na taratibu za maombi hayo zitatolewa katika vyombo vya habari.