Serikali yataka uwekezaji kwenye fukwe

0
71

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa viongozi, wataalamu na wawekezaji kujadili namna bora ya kutunza, kusimamia na kuwekeza katika fukwe zilizopo nchini.

Makamu wa Rais amesema hayo mkoani Mwanza alipokuwa akifungua Jukwaa la Nane la Maendeleo Endelevu, lenye dhima ya Usimamizi Madhubuti wa Fukwe kwa Maendeleo endelevu.

Amesema unahitajika ubunifu katika kutumia zaidi ya kilomita 1,400 za ukanda wa Pwani ya bahari na fukwe safi, hifadhi tatu za baharini, maeneo tengefu ya baharini 15, maziwa na mito mikubwa ambayo inaongeza idadi ya fukwe ambazo bado hazijaweza kutumika kikamilifu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Aidha, Makamu wa Rais amesema serikali imeweka mkazo katika kuendeleza uchumi wa Buluu pamoja na suala la hifadhi na usimamizi wa mazingira nchini.

Ameagiza kila mkoa kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira pamoja na wadau wengine kuharakisha mchakato wa kuandaa mpango utakaoainisha namna ya kufanya uwekezaji wa kuendeleza fukwe zilizopo nchini pamoja na bustani za kupumzikia.