Serikali yataka uwazi uendeshaji taasisi za dini

0
278

Rais Samia Suluhu Hassan ametaka kuwepo kwa uwazi katika uendeshaji wa taasisi zinazomilikiwa na madhehebu ya dini, ili kufahamu kama taasisi hizo zinastahili msamaha wa kodi au la.

Rais Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo mkoani Morogoro wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), mkutano ambao pia unachagua viongozi wa Jumuiya hiyo kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

Amesema kwa muda mrefu baadhi ya taasisi zinazomilikiwa na madhehebu ya dini ambazo zimekuwa zikitoa huduma za afya na elimu kwa Wananchi zimekuwa zikiomba kusamehewa kodi mbalimbali, ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan, utekelezaji wa jambo hilo umekuwa mgumu kutokana na kutokuwepo kwa uwazi kama taasisi hizo.zinatoa huduma bure ama kibiashara.

Amesema wakati umefika kwa taasisi hizo kuwa wazi, na kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika; ili ifahamike ni zipi ambazo zinastahili kusamehewa kodi na zipi ambazo zinatakiwa kuendelea na shughuli zake kibiashara.

Rais Samia Suluhu Hassan ameipongeza Jumuiya hiyo ya Kikristo Tanzania kwa kuendelea kushirikjana na Serikali katika kutoa huduma mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na elimu na afya.