Serikali yataka utulivu sekta ya usafirishaji

0
127

Wakuu wa mikoa iliyopo mipakani wameagizwa kufanya ufuatiliaji wa watu waliounda vikundi visivyo rasmi, vinavyosababisha migogoro katika sekta ya usafirishaji.

Agizo hilo limetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alipofanya ziara ya kawaida ya kukagua mwenendo na shughuli za usafirishaji katika halmashauri ya mji wa Tunduma mkoani Songwe.

Akitoa agizo hilo Waziri Mkuu Majaliwa amesema, Serikali haitomvumilia mtu yeyote anayejihusisha na vitendo hivyo vilivyo tofauti na sheria na taratibu za nchi.

“Ukifanya vitendo viovu utajiingiza kwenye migogoro, kuwa makini usijeingia kwenye mgogoro kwa kutumwa tu, tunazo sheria za nchi.” ameonya Waziri Mkuu

Amesema iwapo kuna changamoto yoyote katika sekta ya usafiri inayowahusisha madereva na waajiri wao, wasisite kuziwasilisha Serikalini.

“Kama zipo shida njooni sisi tutawapokea na kuwasikiliza ili kutatua shida zenu, malori yanayotoka na kuingia nchini yaachwe, tusijihusishe na migogoro ambayo inatatulika.” amesema Waziri Mkuu Majaliwa