Serikali yataka kuboreshwa huduma za maabara

0
397

Serikali imewataka wanataaluma ya maabara kuboresha ubora wa huduma za maabara ili kuwezesha upatikanaji wa matokeo sahihi ya uchunguzi wa magonjwa yatakayowawezesha wananchi kujua afya zao pamoja na kupata matibabu sahihi.


 
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel alipomwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye ufunguzi wa kongamano la 35 la kisayansi la wataalam wa maabara lililofanyika mkoani Dar es Salaam.
 
Dkt. Mollel amesema kipaumbele cha sekta ya afya kwa sasa ni ubora wa huduma, hivyo kuwasisitiza wataalam hao kufanya kazi kwa ufanisi na kuboresha huduma wanazotoa.
 
“Watu wa maabara mkikosea matokeo yake yanaonekana mara moja na wakati mwingine yanagharimu maisha ya watu, Waziri Mkuu amewaomba mkifika kwenye maeneo yenu ya kazi mkasimamie ubora wa huduma kwa sababu maisha yetu yapo mikononi mwenu.” amesema Dkt. Mollel
 
Aidha amesema serikali imepokea changamoto iliyowasilishwa ya masuala ya kimuundo wa utumishi wa kada ya wataalam wa maabara na kuahidi kufanyiwa kazi kwa suala hilo.