Serikali yatahadharisha homa ya manjano

0
149

Serikali kupitia Wizara Afya inaendelea kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa watu wenye dalili za ugonjwa wa homa ya manjano katika vituo vya afya vya bandari, viwanja vya ndege na mipakani kwa wasafiri watokao nje ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati wa mkutano wake na Waandishi wa habari.

Amesema hatua nyingine inayochukuliwa na Serikali ni kuhakikisha Wasafiri wanaotoka nchi zenye hatari ya ugonjwa wa homa ya manjano  wanakuwa na uthibitisho wa chanjo dhidi ya ugonjwa huo kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini. 

Waziri Ummy Mwalimu ametoa kauli  hiyo ikiwa zimepita siku chache baada ya  wizara ya Afya kupokea taarifa kutoka ofisi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyopo nchini, ikielezea kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa homa ya manjano nchini Kenya katika jimbo la Isiolo.

Ugonjwa wa homa ya manjano husababishwa na virusi ambavyo huenezwa na mbu aina ya Aedes, kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na vilevile kati ya mtu na mtu.

Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na homa, kuumwa na kichwa, maumivu ya misuli pamoja na mgongo, mwili kutetemeka, kupoteza hamu ya kula, kusikia kichefuchefu na kutapika, mwili kuwa na manjano, kutokwa na damu sehemu za wazi kama mdomoni, puani, machoni na tumboni na wakati mwingine damu huonekana kwenye matapishi na kinyesi na ugonjwa unapokuwa mkali figo hushindwa kufanya kazi.

Wizara ya Afya imewataka Wananchi wote kujikinga na homa ya manjano ikiwa ni pamoja na kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa na  kuutilia mkazo usafi wa mazingira na kuzuia maji yasituame hovyo kwenye mazingira ili kuangamiza mazalia ya mbu.