Serikali yasema haijazuia biashara ya mazao ya misitu

0
300

Wizara ya Maliasili na Utalii imesema  haijazuia biashara ya mazao ya misitu huku ikiwataka wafanyabiashara wa mazao ya misitu  kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha kunakuwa na usawa katika biashara hiyo pamoja na matumizi endelevu ya rasilimali hiyo.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kibaha Vijijini, Michael Mwakamo aliyetaka kujua kauli ya Serikali juu ya Wafanyabiashara wa mazao ya misitu wanaozuiwa kufanya biashara na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

”Natoa rai kwa wafanyabiashara wote wenye nia njema ya kuvuna au kufanya biashara ya mazao ya misitu wafuate sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa,” Masanja amesisitiza.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Agnes Marwa kuhusu Serikali kuwatafutia eneo mbadala wananchi wa vijiji vya Kata ya Nyantwari – Bunda wanaofanyiwa uthamini kupitisha uhifadhi Masanja amesema kuwa zoezi la uthamini lipo katika hatua za mwisho na baada ya hapo Wananchi watalipwa fidia kwa mujibu wa sheria itakayohusisha gharama za thamani ya ardhi, mazao, majengo, posho ya kujikimu, usafiri na posho ya usumbufu.

Amesema Serikali kupitia Halmashauri ya Mji wa Bunda imetenga na kupima viwanja 350 katika eneo la Virian Kata ya Stoo ambapo Wananchi watakaohama kutoka Kata ya Nyantwari watapewa kipaumbele wakati wa uuzaji wa viwanja hivyo.