Pongezi hizo zimetolewa leo jijini Dar es Salaam na mwakilishi wa Ubalozi wa Pakistani hapa nchini Muhammad Saleem wakati akikabidhi vifaa vya kujikinga na ugonjwa huo kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Saleem anasema tangu ugonjwa huo ulipoingia hapa nchini mwezi uliopita kasi ya maambukizi ni ndogo ukilinganisha na nchi zingine, hiyo yote ni kutokana na hatua thabiti zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Mwakilishi huyo wa Ubalozi wa Pakistani ameishauri Serikali kuendelea kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii katika kutoa elimu ya ugonjwa wa COVID-19 ili wananchi waendelee kupata elimu ya kutosha ambayo itawasaidia kujikinga na ugonjwa huo.
Kwa upande wake mganga mkuu wa Serikali, Prof. Muhamad Kambi ameushukuru Ubalozi wa Pakistani kwa msaada walioutoa na kusema kuwa utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Prof. Kambi amesema ugonjwa wa COVID -19 ni janga la dunia, watu wengi wamepata madhara kutokana ugonjwa huo hivyo basi hakuna msaada mdogo. “Msaada wowote unaotolewa kwa Serikali utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na ugonjwa”.
Ubalozi wa Pakistani umetoa msaada wa barakoa za upasuaji 1800, kofia ambazo zinavaliwa na wahudumu wa afya wakati wanahudumia wagonjwa 1800, kava za viatu za kuvaliwa wodini 800, barakoa za N95 zipatazo 500, magauni ya kuvaa watoa huduma za afya 100, glovu 8000 pamoja na miwani ya kujikinga na virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona 60. Thamani ya vifaa hivyo ni zaidi ya shilingi milioni 11.