Serikali yapiga marufuku mikusanyiko isiyo ya lazima

0
201

Serikali imepiga marufuku mikusanyiko yote isiyo ya lazima nchi nzima, na kuagiza ile ambayo itaonekena ni lazima basi tahadhari zote dhidi ya corona zichukuliwe.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amesema hatua hiyo inalenga kukabiliana wimbi la tatu la maambukizi ya virusi vya corona, ambalo madhara yake yanaendelea kujitokeza.

Katika taarifa hiyo, Waziri Gwajima amewataka Viongozi wa Serikali na wale wa sekta binafsi kuonesha mfano wa namna wanavyochukua hatua kukabiliana na ugonjwa wa corona.

Kwa mujibu wa Dkt. Gwajima, idadi ya wagonjwa wa corona imezidi kuongezeka nchini, na hadi kufikia tarehe 21 mwezi huu kulikuwa na wagonjwa 682 wanaopatiwa matibabu kwenye vituo mbalimbali vya kutolea huduma.

Pia amewataka Wananchi wote kujiandaa kupata huduma ya chanjo dhidi ya corona, ambayo itatoewa bure na kwa hiari.

Amesema leo Julai 22 Wataalamu wa afya wamekutana
kupata mafunzo, tayari kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa huduma ya chanjo dhidi ya corona, na kwamba taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.