Serikali yakunjua makucha vitendo vya rushwa ya ngono

0
209

Serikali imesema haitavumilia vitendo vya rushwa ya ngono katika taasisi za elimu kwani ni ukosefu wa maadili na vinashusha heshima ya wanataaluma pamoja na taaluma katika taasisi hizo.
 
Kauli hiyo imetolewa mkoani Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati akizindua siku ya afya ya akili iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo amesema vitendo hivyo vinapaswa kukemewa kwa nguvu zote na kuchukuliwa hatua mara moja pale inapobainika mtumishi yeyote ameshiriki vitendo hivyo.
 
Waziri Ndalichako amewataka wanafunzi wa kike katika taasisi za elimu wanapokutana na kadhia ya rushwa ya ngono kutokukubali kuingia katika mtego huo na badala yake watoe taarifa kwa idara na vitengo vinavyohusika na ushauri na unasihi katika taasisi hizo ili hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa wahusika.
 
“Sisi kama serikali tunasikitika sana tunapoona na kusoma katika vyombo vya habari taarifa za watoto wetu wa kike katika taasisi za elimu wananyanyasika kwa vitendo hivi vya rushwa ya ngono, nawaomba sana binti zetu msisite wala kuogopa kutoa taarifa ili tuweze kuchukua hatua za kinidhamu kwa wahusika na kuwalinda msikubali kunyanyasika kwa ajili ya maumbo yenu,” -amesisitiza Waziri Ndalichako.
 
Aidha, Waziri Ndalichako amekipongeza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuanzisha Kitengo cha Ushauri na Unasihi chini ya Kurugenzi ya Huduma za Jamii kwa nia ya kuwasaidia wafanyakazi na wanafunzi kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo msongo wa mawazo, sonona, utendaji kazi chini ya kiwango, utoro na ukiukwaji wa miiko na maadili ya kazi.