Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amevitaka vyuo na taasisi zinazotoa taaluma ya uandishi wa habari kufanya tathmini ya mchango wao katika kukuza na kuendeleza tasnia ya habari nchini.
Waziri Nape ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam wakati akifungua kongamano la maadhimisho ya miaka 60 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kongamanno lililolenga kuangalia mchango wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC).
Amesema tathmini hiyo ambayo inapaswa pia kuhusisha wadau wa habari, itasaidia kujua mahitaji ya wanataaluma wanaohitajika kwenye soko.
Akizungumzia kongamano hilo, Waziri Nape amesema tathmini na makongamano ya aina hiyo yatasaidia kuona uhitaji uliopo mtaani na kufanya mabadiliko ya mitaala kulingana na uhitaji.
Amesema serikali inafanya juhudi kubwa kufungua fursa mbalimbali zinazolenga kuboresha tasnia ya habari, lakini bado kuna changamoto kadhaa.
Amezitaja changamoto hizo kuwa ni.pamoja na tasnia ya habari kutokuwa na hadhi inayostahil, hali inayosababisha wasio wanataaluma kuvamia jambo ambalo halikubaliki.