Serikali yaingia mkataba wa kuiuzia matunda kampuni ya Bakhersa

0
778

Ofisi ya waziri mkuu imeingia mkataba na Bakhresa Group of Companies inayohitaji kati ya tani 40,000 na 60,000 za maembe na ukwaju, ambapo vijana watanufaika kwa kupata masoko ya bidhaa zao.

Naibu Waziri wa Ajira, Kazi, Vijana na Walemavu, Anthony Mavunde amesema kampuni hiyo ya mfanyabiashara maarufu nchini Said Bakhresa kuingia mkataba kununua bidhaa hizo za matunda ni fursa nzuri kwa vijana kuichangamkia kwani soko la uhakika lipo.

“Vijana 15,000 kwa kuanzia watapata fursa hii ya kuuza mazao yao ya matunda ya embe na ukwaju kwa kampuni ya Bakharesa, ambayo inauhitaji wa tani 40,000 mpaka 60,000 wa bidhaa hizo kila mwaka,” alisema Mavunde.

Amesema kupitia uwekezaji mkubwa unaofanywa na Bakharesa hapa nchini kupitia bidhaa hizo ameweza kutoa ajira 3,000 mpaka 6,000.

“Katika kipindi hiki cha kuelekea Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati sekta ya kilimo, ni sekta muhimu sana kwa kuwa ndiyo inayotegemewa katika uzalishaji wa malighafi ya viwanda hivyo ni wajibu wa vijana kuchangamkia fursa na halmashauri zote nchini kupitia majiji, manispaa na wilaya zifanye mchakato wa kuunganisha vijana hao ili wapate kunufaika na fursa hii adhimu.”